Thursday, February 16, 2017

MABANDA BORA YA KUKU

Image result for MABANDA BORA YA KUKU

Ujenzi wa mabanda bora ya kuku ni miongoni mwa mambo ya msingi kabisa katika ufugaji bora wa kuku wawe ni wa asili au wale walioboreshwa. Hata hivyo si kila mtindo wa ujenzi unafaa, kwahiyo ujenzi huo ni lazima uzingatie mahitaji halisi ili ufugaji huo uweze kutoa matokeo bora yanayotarajiwa na mfugaji.
Image result for MABANDA BORA YA KUKU
Mambo muhimu katika ujenzi wa banda la kuku ni;
1.      Liingize hewa safi wakati wote.
2.      Liwe kavu daima.
3.      Liwe nafasi ya kutosha.
4.      Liwe la gharama nafuu lakini la kudumu.
5.      Lizuie kuingia wanyama na wadudu hatari kwa kuku.
6.      Liwe na nafasi ya kuweka vyombo vya chakula na maji.
7.      Lizuie upepo wakati wa baridi kali.
Image result for MABANDA BORA YA KUKU
 HEWA NA MWANGA:

 Hewa ni muhimu kwa kila kiumbe, hivyo banda la kuku ni lazima liingize hewa safi na kutoa ile chafu na liweze kuingiza mwanga wa kutosha.
1.      Kwa kifupi ni kwamba madirisha ya banda ni lazima yawe makubwa na ya kutosha ili yaingize hewa safi na kutoa ile chafu.
2.      Ni vema madirisha haya yawe juu kiasi cha meta moja (1) kutoka chini ili hewa ipite juu ya vichwa vya kuku.
3.      Hewa safi siyo upepo, hivyo jaribu kuzuia upepo mkali kuingia ndani ya banda la kuku ama sivyo kuku wataugua ugonjwa wa mafua na niumonia na vifaranga vinaweza kufa  kwa ugonjwa wa baridi.
4.      Jenga   Banda lako kwa kukinga upepo unakotokea na kupanda miti kuzunguka banda hilo la kuku ili kupunguza kasi ya upepo na kuweka kivuli dhidi ya jua kali na joto.

UKAVU NA USAFI WA NDANI:

Kwa vile kuku si ndege wa majini kama bata , ni jambo la busara kuhakikisha kuwa mahali anapoishi hapana unyevunyevu.
§  Banda la kuku lijengwe mahali palipoinuka ili kuzuia maji ya mvua yasiingie.
§   Wajengee kuku uchaga wa kulalia kwa kuweka viguzo vyenye urefu wa meta moja na kutandika miti juu yake ili usiku walale hapo, kuliko kuwalaza ardhini au sakafuni.
§  Ukavu wa banda ni muhimu sana hasa kwa vifaranga na kuku wanaotaga. Ndani ya banda lenye unyevu mayai kuchafuka sana hata wakati mwingine huoza kwa urahisi na jitihada zako zitakuwa ni bure.
§  Sakafu ya banda ni vizuri ikawa ya zege lakini kutokana na uhaba wa fedha sakafu inaweza kutengenezwa kwa mabanzi (mabanda yaliyoinuliwa) au udongo mgumu na au mchanga ambao utafunikwa kwa mabaki ya taka za mpunga na yale ya mbao. 
§  Ili kuepuka unyevunyevu ni vyema eneo/mahali pla kujenga banda pawe pameinuka na penye kupitisha hewa ya kutosha.

PAA LA BANDA:
Image result for MABANDA BORA YA KUKU

Paa la banda liwe madhubuti ili kuzuia maji ya mvua kuingia hasa wakati wa masika. Sakafu ya banda iwe juu zaidi ya usawa wa nje. Paa linaweza kuezekwa kwa mabaki ya vipande vya bati , madebe na kama ikishindikana tumia nyasi zinazofaa kwa ajili ya kuezeka nyumba katika eneo hilo.

NAFASI YA KUFANYA KAZI:

Banda la kuku lisiwe na nguzo au mbao nyingi sana ndani kiasi cha kumfanya mhudumiaji wa kuku ashindwe kufanya kazi zake. Hali hiyo itamfanya apoteze muda mwingi katika kuzizunguka nguzo hizo, hasa wakati wa kuokota mayai au kufanya usafi.

VIFAA:

Unapotaka kujenga banda la kuku kwanza kabisa tayarisha vifaa vinavyotakiwa. Vitu kama miti au nyasi, nyavu au fito, misumari au kamba ni muhimu kuviandaa mapema.
Pili ni lazima uwe na plani/ramani kamili ya banda hilo. Kwa wastani kila kuku anahitaji nafasi ya Meta za eneo la 0.11 hadi 0.22 (futi 1 hadi 2 za eneo.) kutegemeana na umri wa kuku.

UJENZI RAHISI:

Kuku wafugwao hatimaye ni lazima wafidie gharama za Ujenzi wa mabanda na chakula. Gharama zikiwa kubwa sana huenda ukaifanya shughuli ya ufugaji isiwe na faida hata kidogo hali hiyo itamfanya mfugaji aone ufugaji hauna maana yoyote kwake. Lakini ukijenga banda lako kwa kutumia vifaa vinavyopatikana kwa urahisi utaongeza faida zaidi kwakuwa umepunguza gharama za uendeshaji wa mradi.

VIPIMO:

  Banda la kuku linatakiwa liwe na Meta 15 hadi meta 22 za eneo yaani Meta 3 hadi 4.5 za upana kwa meta 5 za urefu. Banda hili linaweza kutunza kuku 100 wakubwa kwa wakati mmoja.

HITIMISHO;

·         Ujenzi wa mabanda unasisitizwa katika kuboresha ufugaji wa kuku wa asili ili;
·         Kuongeza uzalishaji na kupunguza vifo vya vifaranga kwa majanga mbalimbali kama vicheche ,mwewe, mapaka, mbwa na wizi wa kuku wanaozurura holela.
·         Vile vile inatarajiwa kwamba kuku wanaozuiliwa kwenye banda na kuwekewa chakula mchanganyiko wataongeza uzalishaji kwa kiasi kikubwa.

UTAGAJI NA UATAMIAJI WA MAYAI:

a.       Kuku huanza kutaga wakiwa na umri wa majuma 22-32 baada ya kuzaliwa kutegemeana na ukoo ,afya na lishe.Kwa kawaida kuku wa kienyeji /asili watachelewa kutaga kuliko wa kisasa . Matetea hufikia kiwango cha juu cha utagaji wakiwa na umri wa wiki 40-50 na baada ya umri huo utagaji huanza kupungua kidogokidogo. Hali hiyo inapoanza kujitokeza wafugaji wanashauriwa kuuza au kuchinja kuku waliofikia umri huo.
b.      Kuku wanaotaga ni lazima wapate chakula chenye madini ya chokaa ya kutosha. Chakula hiki kinaweza kuboreshwa kwa kuongezewa maganda yaliyosagwa ya mayai na ya konokono
c.       wapatie viota vya kutagia katika mabanda yao , kwa njia hii ni rahisi kuyapata mayai na pia mayai yanakuwa safi. ilikuwafundisha kuku kutaga kwenye viota unaweza  kuweka mayai machache katika kiota au mawe yanayofanana na mayai . kuku wanapoaanza kuatamia hukoma kutaga , kutokana na kuokota mara kadhaa kwa siku unaweza kuepuka kuku kutaka kuatamia .unashauriwa kutenga mara moja matetea wanaoanza kuatamia
kwa kuwaweka katika kibanda kidogo kilichotulia akae pekee yake sehemu isiyo na kiota kwa siku chache.
d.      joto la kadri kwa kuku wanaotaga ni kati ya 18ºC -29ºC.

Mauzo ya mayai:
1.      Hakikisha unafanya utafiti kabla ya kuanza kufuga.
2.      Uza  mayai  kwa kuzingatia viwango kama vile rangi, ukubwa  na maumbile yake.
3.      uza mayai safi kwa kuhakikisha unapanga mayai safi kwenye trei na yale ambayo ni machafu unayasafisha kwa kupanguza na pamba au kitambaa kilicholowekwa maji yasiyo na sabuni( kitambaa kisiwe kimetota maji). Mayai haya yasafishwe kabla ya kuuzwa.
4.      Punguza uvunjaji  na uchafuzi wa  mayai. Hii inawezekana tu pale utakapohakikisha unatengeneza viota vya kutagia na kuyaokota mara kwa mara. Inapendekezwa uokote mayai mara tatu kwa siku. Asubuhi wakati kulisha mchana na jioni. Kuvunjika kwa mayai huongeza hasara kwa mradi na kuchafua matrei ya kutunzia .

Kuatamia.

Mayai ya kuku huanguliwa kwa siku 21 kabla ya vifaranga kutotlewa  ilhali bata  hutotoa baada ya siku 28.

Uatamiaji wa asili na utotoleshaji vifaranga:

Mayai kwa ajili ya kuatamiwa ni lazima yawe mapya;
1)      Umri wa mayai baada ya kutagwa usiwe zaidi ya siku kumi (10) na yawe yamehifadhiwa katika sehemu yenye ubaridi usozidi nyuzi joto 20ºC .Iwapo hali ya joto iko juu kuliko 20ºC basi mayai ya kutotoa vifaranga yasihifadhiwe kwa zaidi ya siku tano (5).
2)      Ili kupata matokeo mazuri, mayai ya kuatamiwa (mayai yaliyochaguliwa) yanatakiwa yawe na umbo la kawaida na ukubwa wa wastani kwa aina ya kuku wanaohusika.
3)      Ganda la mayai ya kuangua lisiwe na mikwaruzo au nyufa  kwani likiwa na nyufa yai hupoteza unyevunyevu ambao ukipungua kiiini cha yai kinaweza kufa au linaweza kuingiza vimelea kama fangasi na bakteria ambavyo husababisha kutotolewa kwa vifaranga vyenye afya mbaya au vilivyokufa.
4)      Hifadhi mayai ya kuangua kwenye makasha makavu ndani ya shimo lililopo ardhini katika sehemu yenye ubaridi kuliko sehemu zote ndani ya chumba.
5)      Kabla mayai hayajaatamiwa chunguza mayai ambayo yana mbegu na yale yasiyo na mbegu . Mayai ya kuku aliyepandwa na jogoo yanakuwa na mtandao wa mishipa ya damu mapema sana ambayo inaweza kuonekana kwa kutumia mwanga mkali wa kurunzi.
6)      Kabla mayai hayajaatamiwa chunguza mayai ambayo yana mbegu na yale yasiyo na mbegu . Mayai ya kuku aliyepandwa na jogoo yanakuwa na mtandao wa mishipa ya damu mapema sana ambayo inaweza kuonekana kwa kutumia mwanga mkali wa kurunzi.
7)      Baada ya mayai kuatamiwa kwa siku saba hadi kumi yanaweza kuchunguzwa mayai yasiyorutubushwa na yenye viini vilivyokufa yanaweza kutambuliwa katika siku saba baada ya kuanza kuanguliwa
8)      Wakati wa kupima kwa kutumia mwanga wa kurunzi mayai yaliyorutubishwa yanakuwa na mishipa ya damu inayoonekana, na doa jeusi ambalo ndicho kiini cha uhai.
9)      Iwapo kiini cha uhai kimekufa, kinaoonekana kama kitu cha mviringo mfano wa pete kuzunguka kiini hai.
10)  Mayai ambayo hayajarutubishwa yanakuwa na nafasi kubwa ya hewa na kiini cha uhai kinaoonekana kama kitu cheusi ndani ya ndani ya yai.
  Mayai ambayo hayajarutubishwa na yale yenye viini vilivyorutubishwa inabidi yatengwe na kuondolewa ili yasije yakaozea ndani ya kiota, yakapasuka na kuharibu mayai mazuri ambayo yapo katika kuatamiwa.

Kiota cha kuku anayeatamia;

1)      Kuku anayeatamia atengwe katika kundi ili asisumbuliwe na kuku wengine ,
2)      Mtengee kuku kiota ambacho kinampa nafasi ya kupata maji safi na chakula kwa karibu.
3)       Kiota au kikapu ni lazima kiwe kikubwa kiasi cha kumpa kuku nafasi ya kuatamia mayai yote.
4)      Weka matandazo makavu ambayo ni mapya yaliyonyunyizwa majvu kidogokuzuia visumbufu.
5)      Iwapo vifaranga wanaototolewa ni wachache njia nzuri ya kuatamia mayai ni kumtumia kuku kuliko mashine ya kutotolesha vifaranga kwasababu kuku ana uwezo mkubwa wa kutotoa vvifaranga  kwa asilimia 80- 100 ukilinganisha na mashine ambayo hutotoa mayai kwa asilimia 60-80 tu.
Vifaranga  vikishatotolewa vinaweza kulelewa kwa kumtumia mama ikiwa ni wachache. Lakini vifaranga wanaweza kulelewa kwa kutumia kifaa maalum ya kulelea vifaranga.

LISHE YA KUKU NA KUCHANGANYA CHAKULA


 LISHE YA KUKU:
Image result for KUCHANGANYA CHAKULA cha  KUKU
Ili kuku waweze kuishi, kukua vizuri, kunenepa na kutaga mayai mengi ni lazima wale chakula kingi na chenye ubora unaotakiwa. Uwingi na ubora wa lishe ya kuku unaweza kuainishwa katika makundi ya vyakula kama ifuatavyo:
1.      Vyakula vya kutia nguvu
2.      Vyakula vya kujenga mwili
3.      Vyakula vya kuimarisha mifupa
4.      Vyakula vya kulinda mwili
5.      Maji.

Makundi ya vyakula:

    1. Vyakula vya kutia nguvu:

Vyakula vya mifugo vifuatavyo vinawekwa katika kundi hili;
a.       Pumba za mahindi, pumba laini za mpunga, na, pumba laini za ngano.
b.      Nafaka kama vile mtama , chenga za mahindi ,chenga za mchele, uwele , na ulezi
c.       Mimea ya mizizi kama vile muhogo, viazi vitamu na magimbi. Kabla ya kulisha kuku hakikisha mizizi hiyo inalowekwa kwa muda wa saa moja au kupikwa kabla ya kukausha ili kuondoa sumu ambayo kwa asili imo katika vyakula vya aina hii.Inashauriwa kuwa  mizizi hiyo ilishwe kwa kiasi cha asilimia 10% ya chakula chote anacholishwa kuku.
 Katika kundi hili la kutia nguvu ,vyakula vya mafuta kama vile mafuta ya kutoka kwenye vyakula vya mafuta kama mashudu ya mimea ya mafuta, mafuta ya samaki husaidia kuongeza nguvu na joto mwilini. Vyakula vya kutia nishati huchangia asilimia 60-70 ya mchanganyiko wote wa chakula.

1.        Vyakula vya kujenga mwili:
  Mashudu :Haya ni makapi ya mbegu za mimea aina ya mikunde na vyakula v vinavyotoa mafuta kama vile alizeti, mawese, karanga, soya ,korosho, na ufuta .
  Damu ya wanyama iliyokaushwa (waliochinjwa na kukaguliwa), hii inafanywa ili kuepusha uwezekano wa kuku kupata magonjwa ya kuambukiza .
  Mabaki ya samaki ya samaki/dagaa na nyama.
  Vyakula asilia kama vile minyoo, mayai ya mchwa, Masalia ya nyama toka kwenye ngozi/mifupa, wadudu walioteshwa kutokana na damu au nyama iliyooza na vyakula vya aina nyingine.
  Vyakula hivi huchangia asilimia 20 hadi 30% ya mchanganyiko wote wa chakula cha kuku.

2.   Vyakula vya kuimarisha mifupa(madini): a)Hivi ni vyakula vya madini ambavyo huhitajika kwa ajili ya kujenga mifupa, maganda ya mayai, kukua na kuuweka mwili wa ndege (kuku) katika hali ya afya njema kwa ujumla.
b)      Madini ya muhimu ni madini ya chokaa (calcium) na fosiforasi (phosphorus). Ili kuku watage mayai yenye ganda gumu ni lazima wapate madini ya chokaa maganda ya konokono na mayai yaliyosagwa vizuri. Lakini inapendekezwa kwamba unapoongeza madini ya fosforasi inakubidi uongeze pia madini ya chokaa kadri inavyopasa ,kwasababu kiwango cha aina moja kikizidi kuliko cha aina nyingine husababisha upungufu wa kile kidogo
Viinilishe vya madini vinavyotakiwa ni pamoja na;
  Majivu ya mifupa yaliyosagwa vizuri, unga uliosagwa wa magamba ya konokono wa baharini, konokono wa nchi kavu na maganda ya mayai yaliyochomwa . Kabla maganda ya mayai na nyumba za konokono havijatumika inashauriwa yachomwe moto mkali au yachemshwe ili kuua vijidudu vya maradhi.
  Chumvi ya jikoni
  Madini yaliyotengenezwa viwandani kama vile Di-calcium phosphate
  Magadi (kilambo).

 4.      Vyakula vya kulinda mwili:
Kundi hili linajumuisha vyakula vya mbogamboga kama vile;
Ø  Mchicha, samadi ya ng’ombe ambayo haijakaa muda mrefu baada ya kunyewa, mchicha pori, Chinese kabeji n.k.
Ø  na Mchanganyiko wa vitamini uliotengenezwa na viwanda vya madawa (vitamin premix).
Ø  Jua ni muhimu katika kuhakikisha vitamini A na D zinatumika vizuri mwilini, kwahiyo banda ni lazima lijengwe kwa mtindo ambao unaruhusu mwanga kupita hasa nyakati za asubuhi na jioni.
Ø  Chakula cha kuku wanaofugwa ndani ni lazima kichanganywe na vitamini zinazotayarishwa viwandani.

          KUCHANGANYA CHAKULA CHA KUKU:

Njia za kuchanganya chakula cha kuku;
Kuna njia kuu mbili za kuchanganya chakula cha kuku, nazo ni;
 Kuchanganya chakula kwa mashine;
o   Njia hii hutumika viwandani kuchanganya chakula kwa ajili ya kuku wanaofugwa katika mashamba makubwa.
  Kuchanganya chakula majumbani (home made ration): Hii ni njia inayotumika kuchanganya chakula kwa ajili ya kulisha kundi dogo la kuku na njia ambayo inaweza kutumiwa na wafugaji wadogowadogo.
VIFAA; Beleshi /koleo(spade), Turubai/sakafu safi, Viinilishe , Viroba/Magunia kwa ajili ya kuhifadhia chakula kilichochanganywa.
Chakula kilichochanganywa kinaweza kuwekwa katika uzani wa kilo 25-kilo 50, au kilo 100.

 MCHANGANUO WA VIINILISHE VYA CHAKULA CHA KUKU:

 
Aina ya chakula                                   kiasi
i.                    Vyakula vya kutia nguvu mwilini:
Ø  Pumba za mahindi            kilo   48
Ø  Pumba laini za mpunga    kilo   26
            Jumla                                            kilo 74

  ii.            Vyakula cha kujenga mwili : 
                                       

    Mashudu ya alizeti                                   kilo 18

        Damu ya wanyama                                                                    kilo   1
        Mabaki ya samaki /dagaa                                                          kilo   3

          Jumla                                              kilo  22


iii.Vyakula vya kuimarisha mifupa (Madini):
  1. chumvi ya jikoni                                   kilo ½
  2. chokaa(dicalciumphosphate)…            kilo 2
  3. poultry premix/                                     kilo ½ 
  4.  unga wa mifupa                                  kilo 1
          Jumla                                                      kilo 4
  
Ø  Mahitaji halisi ya viinilishe kwa muhtasari:

Ø  Vyakula kutia nguvu mwilini                             kilo 74
Ø  Vyakula vya kujenga mwili                              kilo 22
Ø  Vyakula vya kuimarisha mifupa (Madini)        kilo 4
  JUMLA                                                                        100
Jumla ya mchanganyiko wa vyakula                kilo 100 

 

HATUA ZA KUCHANGANYA CHAKULA CHA KUKU:


HATUA YA KWANZA:

Katika hatua ya kwanza utaanza kuchanganya vyakula vya madini
Changanya , chokaa, chumvi na majivu ya mifupa pig mix vizuri - huu utauita mchanganyo Na.1

HATUA YA PILI:

Changanya mchanganyo huo na damu pamoja na samaki waliosagwa - huu utauita mchanganyo Na. 2

 HATUA YA TATU:

Mchanganyo Na.2 uchanganye na mashudu vizuri ambao utauita mchanganyo Na.3.

HATUA YA NNE:

Mchanganyo Na.3 umwage juu ya rundo la pumba iliyochanganywa (pumba ya mahindi na pumba laini ya mpunga).
o   Chukua beleshi /koleo safi lililo kavu na kulitumia kuchanganya rundo la chakula ili kusambaza viinilishe vizuri.

Mambo ya kuzingatia katika kulisha na kutunza chakula cha kuku:

a) Baada ya kuchanganya chakula kitawekwa kwenye viroba au magunia na kutunzwa ghalani (stoo) hadi pale kitakapohitajika kwa ajili ya kulisha kuku.
b) Hakikisha kuku wanapata lishe kadri inavyopendekezwa na wataalamu.
c)  Chakula kilichochanganywa ni lazima kiwekwe sehemu kavu ili kisiharibiwe na unyevunyevu kama vile kwenye chaga mabanzi yaliyotandazwa juu ya mawe yalipangwa vizuri
d)  Chakula kilichoharibika hakifai kulisha kuku kwani kinaweza kusababisha matatizo ya afya.
d) Chakula kilichochanganywa kinatakiwa kisikae muda mrefu baada ya kutayarishwa.

Vyakula vya ziada:
Ili kuhakikisha kwamba kuku wanapata viinilishe vya kutosha kuku wanaweza kupewa mchwa na mafunza.
Vilevile vitu mbadala aina ya nafaka vinavyopatikana hutegemea sana aina ya mazao yanayolimwa katika eneo husika.

Mbinu za kuotesha mchwa na funza: Funza na mchwa ni chakula kizuri na rahisi chenye viinilishe aina ya protini kwa kuku wanaofugwa kwa mfumo huria unaoboreshwa. Hata hivyo vyanzo hivi vya chakula cha protini huchangia tu vile ambavyo kuku wanatakiwa kupewa.
a.       Inashauriwa uwape vifaranga hao funza na mchwa kwa sababu ndio wanaohitaji protini kwa kiasi kikubwa na cha kuaminika.
Funza na mabuu yanaweza kuoteshwa kwa njia rahisi na kutumika kuboresha chakula cha vifaranga.
      c)   Mafunza na mabuu yanaweza kuoteshwa kwa kutumia damu, viungo vya ndani ya tumbo la ng’ombe pamoja na samadi ya ng’ombe.
d)   Chungu kijazwe maji theluthi moja ya ujazo wake, inzi watakuja na kutaga mayai katika mchanganyiko ambao mafunza walioteshwa wataanza kula mchanganyiko huo.
e)   Baada ya hapo vitu hivi vyote vitachanganywa pamoja katika chungu kimoja kikubwa ambacho kitaachwa wazi wakati wa mchana na kufunikwa wakati wa usiku.
f)    Siku tano baadaye maji yatajazwa kwenye mtungi huo na mafunza yatakusanywa wakiwa wanaelea juu. Baada ya kukusanya waoshe vizuri na maji halafu lisha kuku moja kwa moja.
g)   Kumbuka kuweka chungu kinachooteshwa mafunza kuweka mbali na maeneo ya watu ili kuepuka harufu inayoweza kusumbua watu.

                                                  KULISHA KUKU:  
 
 Makadirio ya chakula cha kuwalisha vifaranga 100/siku moja:

Umri (wiki baada ya kuzaliwa)
Idadi ya
 vifaranga
Kiasi kinachotakiwa
Kwa siku moja(kilo)

1
100
1
2
100
1
3
100
2
4
100
3
5
100
4
6
100
5

Maelezo kwa ufupi  kuhusu kulisha kuku:

  Ni vigumu kukadiria mahitaji ya chakula cha kuku wanaojitafutia chakula, lakini inakadiriwa kuwa kuku mmoja mkubwa wa uzito wa kilo 1-2 anahitaji chakula chenye uzani wa gramu 80-160 kwa siku kwa kuku wanofugwa ndani lakini wale kuku wanafugwa kwa mfumo wa huria nusu huria mahitaji yanakadiriwa kupungua hadi kufikia gramu 30-50 kwa siku .
  Ifahamike pia kuwa kiasi cha chakula hutegemea mahitaji kutokana na uzito na uzalishaji, mfano kuku anayetaga na anayekua wanahitaji chakula kingi zaidi ya wale ambao hawatagi au wamekoma kukua.
  Hakikisha kuku wanawekewa chakula na maji safi kwenye vyombo safi na kubadilisha kila vitakapoisha.

0 comments:

Post a Comment