Thursday, March 2, 2017

UFUGAJI WA KUKU WA KIENYEJI WENYE TIJA

Image result for KUKU WA KIENYEJI
Safari yangu ilianza baada ya kukutana na mhamasishaji aliyenitia chachu kwamba 10 x10 x 10 you become a millionea! Kwamba ukianza na kuku 10 kila mmoja akazaa 10 na hao watoto na mama zao wakazaa kila mmoja 10 unakuwa millionea! Wakubwa kuongea ni rahisi utekelezaji ukawa mgumu sana! Changamoto kuu aipatayo mfugaji wa kuku wa kienyeji ni kuzalisha vifaranga wengi na kuweza kuwakuza! Bila hivyo kundi haliwezi kukua na kukupa kipato cha uhakika!

Safari ya ufugaji niliianza kwa kununua mitetea 30 na jogoo watatu! Ilibidi nisubiri muda hadi kuku waanze kutaga! Muda ukafika kuku wakaanza kutaga kwa fujo sana! Nilikuwa na banda moja tu ambamo kuku wote walikuwa wakilala humo. Nilitengeneza viota vingi kwa ajili ya kuku kutagia. Asubuhi nilikuwa nawafungulia! Changamoto nilizoanza kupambana nazo kwanza kama mjuavyo kuku tofauti walikuwa wanataga kwenye kiota kimoja! Ilipofika wakati wa kuatamia ikawa kila kwenye kiota kimoja kuna kuku kadhaa wamebanana wanaatamia! Hali hii haipaswi kutokea kwani kuku mmoja anaweza kuwa amejilundikia mayai mengi ambayo hawezi kuyapajoto la kutosha na kuku mwingine anakuwa amekaa kando tu hana hata yai moja. Hii ilibadilika ikawa kero kubwa! Nilijua utotoaji unaweza kuathirika sana!

Ili utotoreshe vifaranga vingi kwa wakati mmoja badala ya kutumia incubator, tumia hao hao kuku. Wakianza kutaga kila siku okota mayai na kuyahifadhi mahali salama ili kuku wasiyatie joto! Kuku wengi wanapotaga kwa pamoja hufikia wakati mayai huishatumboni unakuta wamelala kwenye viota wakiwa wameatamia mayai yaliyopo au udongo tu! Kuku anaekuwa amefikia kuatamia utamjua kwani ukimshitua haondoki kwenye kiota. Kuku anaetaga ukimshitua hukimbia! Kwa hiyo kama nimepanga kutotolesha vifaranga 100 kwa mara moja nikishagundua kuwa kuna kuku 8 wameanza kuonesha dalili ya kuatamia hapo husubiri usiku ninawawekea mayai amabayo nilikuwa nimeyahifadhi. Ambapo mimi huwekea kila kuku mayai 15. Kwa hiyo kuku 8 hufanya jumla ya mayai 120. 

Kwa kuwa banda langu ni hilo moja tu kuku wengine wanaoendelea kutaga walikuwa wanaendelea kutagia kwenye viota ambavyo kuku wengine walikuwa wanaatamia! Hali hii ilikuwa inaleta tabu sana kwani ilikuwa si rahisi kutambua mayai mapya na yenye siku nyingi. Kuondoa shida hii nilinunua MARKER PEN (rangi yoyote) na siku ya kuwawekea mayai kuku ili waatamie niliyachora mduara kuzunguka yai ili iwe rahisi kuyatambua mayai mapya. Huo mchoro hauwatishi kuku na hakuna dosari yoyote. Kwa hiyo kila siku jioni ninapokuja kuokota mayai yaliyotagwa nilikuwa pia nakagua kila kiota cha kuku walioatamia na kuondoa mayai mapya. Kumnyenyua kuku anaeatamia na kuondoa yai haileti shida yoyote!
Kuku akifikia wakati wa kuatamia ukamnyima mayai hawa wanatabia kuendelea kung'ang'ania kuatamia, hapo ilibidi kutengeneza JELA! Watu wengine wanambinu tofauti kumwachisha kuku asiatamie! Mbinu ya kumtia kuku stress inafanya kazi nzuri sana! Jela inaweza kuwa ni Tega, au Box kubwa au chumba kidogo kilichopo. Ukimfungia kuku JELA bila maji wala chakula kwa kutwa mbili siku ukimfungulia akili yake huwa ni kutafuta chakula tu hakumbuki kurudi kwenye kiota! Njia hii ilifanikiwa sana na ilifanya kuendesha shughuri zangu bila bughudha! Kuna wakati JELA ilikuwa na kuku kibao hivyo unapaswa kutengeneza kibanda cha JELA. Hawa kuku wakitoka JELA hutaga mapema sana amabapo bila hivyo wangekuwa wanaatamia. 

Pia kuku wakishaatamia kwa muda wa siku 10 nilikuwa nayapima mayai ili kubaini kama kuna mayai yasiyoweza kuanguliwa! Ni rahisi sana kama una Tochi! Ukimulika yai Kwa kulizungushia vidole kiganjani kama ni yai zima linakuwa na giza kama ni yai bovu linapitisha mwanga kama yai lililotagwa siku hiyo! Jinsi ya kuzungushia vidole yai, tengeneza duara kwa vidole vyako na dole gumba kisha pachika yai katikati ya duara ili mwanga wa tochi upenye kwenye yai! Kwahiyo unaweka tochi inayowaka chini ya yai na hii ifanyike gizani au ndani ya chumba chenye mwaga mdogo. Kadri ya yai linavyokaribia kutotolewa ukilimulika huwa na giza zaidi! Ukimulika mayai toa mayai yasiyoweza kutotolewa maana hayo hutumia joto la Mama bure!

Bado ntaendelea kuwaletea makala hii kuhusu ufugaji kuku bado sijamaliza nimeona niwarushie hii kwanza kwa kuanzia. Mwenzenu nilikuwa nahangaika kufukia tanuru la mkaa nimekuta limefunguka! Si mnajua maisha jamani! Vijana tuamke na kujiingiza katika miradi hii soon tutaona mabadiliko

9 comments: